Home | Terms & Conditions | Help

May 19, 2024, 12:04 am

NEWS: KESI YA KINA HALIMA MDEE YAPIGWA KALENDA TENA MPAKA MARCH 2023

Dar es salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imeahirisha usikilizwaji wa kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama, iliyofunguliwa na wabunge wa viti maalum 19 akiwemo Halim Mdee dhidi ya kilichokuwa chama chake Chama cha Chadema, hadi Machi, 2023.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na wabunge hao wakiogozwa na Halima Mdee, imeahirishwa leo Jumanne na mahakama hiyo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, ilipokwenda kwa ajili ya usikilizwaji, baada ya mawakili wa Chadema kuomba ahirisho kutokana na kiongozi wa jopo lao, Wakili Peter Kibatala, kuwa nje ya Dar es Salaam kwa ajili ya kushughulikia kesi nyingine ya mauaji.

Ombi la ahirisho liliwasilishwa na Wakili wa Chadema, Jeremiah Mtobesya, ambapo mawakili wa kina Mdee waliliunga mkono kisha Jaji Mkeha aliahirisha mpaka tarehe 6 hadi 9 Machi, 2023.

Leo Jumanne, kesi hiyo ilikwenda kwa ajili ya usikilizwaji, ambapo Mbunge Viti Maalum, Jesca Kishoa, ilikuwa amalizie kuhojiwa maswali ya dodoso dhidi ya malalamiko yake ya kufukuzwa Chadema na mawakili wa chama hicho.

Katika kesi hiyo, kina Mdee wameishtaki Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiiomba mahakama ifanyie mapitio dhidi ya mchakato uliotumika kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa.