Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 6:55 pm

NEWS: KOCHA WA SIMBA NA WENZAKE WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Dar es Salaam. Watuhumiwa sita akiwemo kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultan (40) wamefikishwa leo Jumatatu Novemba 21, 2022 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za Kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilogramu 34.89.

Washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif, Said Matwiko mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu mbonde (54), mkazi wa kisemvule, John John ‘Chipanda’ (40) mkazi wa Kitunda na Sarah Joseph.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mery Mrio kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mshtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya.

Mwanga alidai Oktoba 27,2022 eneo la Kivule jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walisafirisha dawa za Kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilogramu 27.10.

Alidai katika shtaka la pili Novemba 4,2022 maeneo ya Kamegele Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani washtakiwa hao kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilogramu 7.79.

Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo aliomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine na ada ya maelezo hayo Hakimu Mrio alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote na kesi imeahirishwa hadi Desemba 5,2022