Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 9:45 pm

NEWS: MAKAMISHNA WALIOPINGA MATOKEO KENYA WATOA UFAFANUZI

Makamishna wanne wa tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera, wamesema kuwa matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati yanahitilafu kwasababu zaidi ya kura 140,000 hazikuwekwa kwenye majumuisho ya kura zote yanayoleta asilimia 100.

Makamishna hao Wanne ni pamoja na Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang'aya.

Wanne hao walipinga matokeo hayo ya uchaguzi wa tarehe tisa Agosti na kuahidi kutoa maelezo ya kina kuhusu ni nini haswa kilichotokea wakati wa kuhesabu kura hizo za Urais.

Akizungumza na vyombo vya Habari, makamu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Juliana Cherera amefafanua hoja zao zilizowafanya kufikia uamuzi huo.

Alidai kuwa ukiongeza asilimia kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, jumla hiyo ilifika 100.01%.

Madai hayo yanahitaji kuangaliwa na yanaweza kuwa ni hitilafu ya jumla, lakini Bi Cherera alielezea huu kama ''upuuzi wa kihisabati ambao unapinga mantiki''.

Aliongeza kuwa matokeo ya kura za urais hayaakisi maoni ya makamishna, kwa sababu walipaswa kuyashughulikia kabla ya kutangazwa na hawakuweza kuyaona yote.

Walisema kuwa majumuisho ya asilimia ya kura alizopewa kila mmoja wa wagombea urais wanne ilizidi asilimia 100.

"Jumla hii inatupa jumla ya asilimia 100.01. Hii inamaanisha takriban kura 142,000 ambazo zitafanya tofauti kubwa katika matokeo ya mwisho,'' Cherera alisema.

"Tulipotaka tuhakiki matokeo, mwenyekiti alikataa na kusisitiza kutangaza matokeo," aliongeza.

Aidha makamishna hao walisema walikataa kumiliki matokeo kwa sababu matokeo yanatangaza idadi ya wapiga kura waliojiandikisha, kura zilizopigwa na idadi ya kura zilizokataliwa.