Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 4:58 pm

NEWS: NAIBU WAZIRI ATUHUMIWA KWA KUCHOCHEA MIGOGORO YA ARDHI

Babati. Serekali mkoani Manyara imewatuhumu vikali Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Abdulrahaman Kololi kwa kuhusika kuchochea mgogoro wa ardhi kwenye shamba la Dudumera la Kata ya Maisaka kwa kushawishi wananchi wavamia shamba hilo.

Waziri Gekul ambaye ni mbunge wa Babati mjini na Kololi ambaye ni Diwani wa kata ya Maisaka wanatuhumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara (RC), Makongoro Nyerere kuwachochea wananchii ili wavamie shamba la Dudumera ambalo ni la mwekezaji.

Makongoro akizungumza mjini Babati kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) leo Jumatano, Novemba 30, 2022 amesema Gekul na Kololi wanawachochea wananchi ili wavamie shamba la mwekezaji na kusababisha vurugu.

Amemwagiza kamanda wa polisi mkoa huo, George Katabazi kuwakamata vijana wanaovamia eneo hilo na kutumia mbinu za kipolisi kuwahoji ili wawataje watu wanaowatuma.

"RPC mkawakamate hao vijana kwani mbunge anahusika na diwani anahusika kuchochea mgogoro ni bora akose hiyo nafasi ili uchaguzi ufanyike na tupate Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya mji," amesema Makongoro.

Amesema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kutembelea mji wa Babati na kutoa onyo kwa viongozi kutochochea migogoro ya ardhi ila anashangazwa na viongozi hao kufanya hayo.

Hata hivyo, Kololi amesema yeye hawezi kuzungumzia chochote juu ya shutuma hizo huku Gekul akisema anashangazwa na shutuma hizo kwani yeye amekuwa mpatanishi wa tatizo hilo na siyo kuchochea migogoro ya ardhi.

"Juzi kulitaka kuzuka vurugu pale juu ya mgogoro huo, nilifika na polisi tukawapooza wananchi, leo inakuwaje nasingiziwa kuanziaha mgogoro huo," amehoji Gekul.

Amesema wananchi hao hawajavamia eneo hilo kwani walikuwepo zaidi ya miaka 70 iliyopita hivyo hawapaswi kuondolewa hivi sasa labda wapewe sehemu nyingine ya kufidiwa.