Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 11:58 pm

NEWS: SEREKALI YABAINI MTAHIMIWA BINTI IPTISAM ALIBADILISHIWA NAMBA

Dar es Salaam. Serikali imeifungia Shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha mitihani kwa muda usiojulikana mra baada ya taarifa ya Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani pamoja na taarifa ya Wataalamu wa Miandiko kutoka Jeshi la Polisi kubainika kuwa ni kweli Binti Iptisam na watahiniwa wengine saba walibadilishiwa namba za mtihani katika Shule hiyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo leo akiwa kwenye Ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dar es salaam ambapo amesema uchunguzi uliofanywa na Wataalamu wa Miandiko katika skripti za Watahiniwa umebaini makosa mengi ikiwemo mwandiko wa Mtahiniwa PS1408009/0033 katika masomo matano kunafanana na wa Mtahiniwa PS1408009/0034 katika somo la sita.

“Uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wataalamu wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi (Forensic Bureau) umebainika jumla ya watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo cha mtihani namba PS1408009 shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic” amesema Profesa Mkenda.

Uchunguzi huo ulifanywa baada kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika Oktoba 05 na 06/10/2022.

Profesa Mkenda amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo Serikali kupitia Baraza la Mitihani ilielekeza Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya mtahiniwa na kuwasilisha taarifa Baraza la Mitihani.

Amesema kuwa uchunguzi uliofanyika pia umebaini kuwa mwanafunzi huyo pamoja na wanafunzi wengine sita walibadilishiwa namba ya mtihani katika mtihani wa taifa wa darasala saba.

“Mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim alifanya masomo matano kwa kutumia namba PS1408009/0040 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0039 na Watahiniwa wengine wanne pia walibadilishiwa namba katika somo la sita katika kituo hicho,” amesema.