Home | Terms & Conditions | Help

May 19, 2024, 12:40 am

NEWS: UKATILI TISHIO CHAMWINO.

CHAMWINO: Ukatili katika wilaya ya Chamwino bado ni tatizo licha ya Serikali na mashirika kuendelea na kampeni ya kupinga.

Takwimu zilizotolewa Desemba 9, 2022 na afisa ustawi wa jamii Wa Wilaya hiyo Deodatus Damian zinaonyesha watu 600 walifanyiwa ukatili, huku kesi 4 zikiwa za ulawiti.

Damian alitoa kauli hiyo katika Mkutano wa hadhara Wilayani chamwino ambao umeandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ActionAid Tanzania na Afnet ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya hiyo bado vipo kwa wingi hali ambayo inahitaji jitihada za makusudi kuvikabili.

“Ukilinganisha na miaka ya Nyuma takwimu zilikuwa chini kwa sababu wananchi walikuwa hawatoi taarifa , kadri tunavyowapa elimu wananchi wanajua ni wapi pakupeleka taarifa hizo, na mkakati mkubwa uliopo ni kuimarisha kamati zetu za ulinzi na wanawake na watoto kwa maana ya (MTAKUWA) Ngazi ya Kijiji , kata na Wilaya,’’ amesema Damian.

Hata hivyo, amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo bado vimeshika kasi katika wilaya hiyo ni Vipigo huku akidai katika matukio ya ulawiti changamoto wanayokumbana nayo ni kukosa ushirikiano kwa wahusika kuripoti na kupelekea kukosa Ushahidi.

Damian ameendelea kusema Kesi nyingi zinakosa Ushahidi kutokana na kumaliza kimila.

Dawati la Jinsia na Watoto polisi Makao Makuu Dodoma Kija Banka amesema kwa sasa wanapata takwimu nyingi za Watoto wa kiume kulawitiwa nakuwataka wazazi kutobweteka nakupaza sauti kuhusiana na watoto wa kiume.

‘’Kesi nyingi sana ni zaulawiti sisi Wanawake tusibweteke kuona sisi tunanyanyasika lakini watoto wetu wa kiume kizazi kijacho watakuwa ni wanawake tutakosa wanaume, Watoto wamekuwa wakilawitiwa mashuleni, sehemu wanazocheza hatujui watoto wanacheza mahala ngani,’’ amesema Banka.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi toka Makao Mkuu Dodoma (SACP), Ulrich Matei amesema ili kupambana na ukatili wa kijinsia njia mbalimbali zitumike mojawapo ni kutoa elimu kwa wananchi kuachana na vitendo vya unyanyasaji ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi.

‘’Nitoe wito ili kubadili mtazamo wa mfumo dume ambao unamfanya mwanaume ajione yeye ndio mwenye mamlaka na nguvu dhidi ya mwanamke,Matukio mengi ya unyanyasaji hutokea kutokana na kukosekana kwa kipato cha kuwezesha kutunza familia,’’

Naye mwenyekiti wa baraza la Watoto Dodoma Wema Nollo amesema Changamoto zinazowakabili watoto ni ndoa za utotoni, ulawiti, ukeketaji ambavyo humpelekea mtoto kukosa vipindi vya shule na kupoteza malengo yao nakuitaka halmashauri kutenga bajeti ili kuandaa mikutano ambayo itajadili changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi.

‘’Pia ningependekeza dawati la jinsia kufika mashuleni kutoa elimu, maana asilimia 60 yaukatili ni majumbani na 40 ni mashuleni,’’ amesema Nollo.