Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 10:29 pm

NEWS: WAKULIMA WAITUPIA JIKO SERIKALI UTAFITI MBOLEA ASILI

DODOMA: Kutokana na wakulima nchini kukabiliwa na Changamoto ya upatikanaji wa mbolea za mashambani, wameiomba Serikali kuzifanyia utafiti mbolea za asili zinayozalishwa na mifugo wakiwemo ng’ombe na mbuzi ili kuepukana na mbolea za kisasa kutoka nje ya nchi.

Wakizungumza katika kikao kilichoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali Action Aid Tanzania na shirika la Policy Forum Jukwaa la Wakulima Wanawake na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe jijini Dodoma, baadhi ya wakulima hao toka baadhi ya mikoa nchini wamesema kero ya mbolea zinaweza kutatuliwa iwapo Serikali itazifanyia utafiti mbolea za asili.

Fredina Saidi mkulima toka Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shiyanga amesema wakulima wengi hususani wanawake wanakabiliwa na tatizo la gharama kubwa la ununuzi wa mbolea hivyo wanaiomba Serikali kuzifanyia utafiti mbolea za samadi ili kuepukana na kuagiza zinatoka nje.

“Iwapo Serikali itakomaa na utafiti wa mbolea zinazotokana na mifugo, inawezekana itaondokana na kero za kelele toka kwa wakulima kununua kwa gharama kubwa mbolea toka nje ya nchi,” amesema Fredina.

Naye Sophia Boke toka wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma amesema wakulima wengi wanashindwa kupata mbolea kwa wakati na inapofika wakulima wengi wanakuwa wapo kwenye mavuno.

“Hivyo ushauri wetu kwa Serikali tunaiomba ituletee mbolea wakati tumeshavuna na kuuza mazao kutokana na kipindi hicho wanakuwa na fedha mkononi…pia zifanyiwe utafiti mbolea za asili,” amesema Sophia.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima Wanawake toka wilayani Chamwino, Janeth Nyamaya, amesema kutokana na kero ya upatikanaji wa mbolea hususani kwa wakulima wadogo wanawake tunaiomba Serikali kuweza kuzifanyia utafiti mbolea za asili zinazotokana na mifugo.

Naye Meneja Mradi wa Action Aid, Samwely Mkwatwa , amesema shirika linawasimamia wakulima wadogo wanawake katika baadhi ya mikoa na kuunda majukwaa yanayoweza kuwasaidia kuzungumzia kero zinazowakabili.

“Kwa mfano hiki kikao shirika limesimamia baada ya wanawake wakulima kuomba kukutana na Waziri kuelezea kero zao…pamoja na kutoonana na Waziri lakini wakurugenzi waliopewa majukumu kusikiliza kero za wakulima zimeonyesha mapokeo,” amesema Mkwatwa.

Hata hivyo, wakizungumza na wanawake wa jukwaa hilo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Usimamizi wa Ardhi ya Kilimo Mhandisi Juma Mdeke amesema Serikali inaendelea kuangalia umuhimu wa mbolea ya samadi na kuendelea kufanyia utafiti.

“Nchi ina teknolojia bora ya kisayansi, tunachoshauri ni kutunza udongo na maji wakati Serikali ikiendelea kufanyia utafiti mbolea za asili kutokana na kufahamu umuhimu wake,” alima Mdeke.

Mkurugenzi wa Mazao Nyasebwa Chimagu amesema atakutana na watu wa Actions aid ili kuweza kusaidia wakulima waweze kuondokana na lindi la umasikini.