Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 9:31 pm

NEWS: WANANCHI KUKOSA HUDUMA YA LUKU KWA SIKU 4

Dar es Salaam. Wateja wa TANESCO ambalo ni Shirika la umeme la Tanzania hawataweza kununua umeme kwa njia ya Luku kwa siku nne, mfululizo kuanzia Agosti 22 - 25, 2022 kuanzia saa 4 usiku hadi saa 1 asubuhi kutokana na matengenezo kwenye kanzidata ya mfumo wa Luku hapa nchini.

Meneja Mwandamizi wa Tehama katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Cliff Maregeli amesema hayo leo Jumatano Agosti 17, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu matengenezo kinga kwenye kanzidata ya mfumo wa Luku.

Ameelezea kuwa matengenezo hayo yanalenga kuongeza ufanisi katika mfumo wa Luku.

Amewataka wananchi kununua umeme wa kutosha katika kipindi hiki kwa sababu hawataweza kununua umeme wa Luku katika kipindi kilichobainishwa.

"Shirika linashauri wateja wake kununua umeme wa ziada au kufanya manunuzi ya umeme nje ya muda wa matengenezo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na kazi hii.

"Matengenezo haya muhimu yanalenga kuongeza ufanisi katika mfumo wa Luku ili kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi zaidi," amesema Maregeli.

Kwa upande wake, Msemaji wa Tanesco, Martin Mwambene amesisitiza kwamba faida kubwa ya matengenezo hayo ni kujihami dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye na matengenezo yakawa makubwa zaidi na kusababisha wananchi kukosa umeme.

"Wananchi wazingatie tu kununua umeme wa kutosha ili waepuke usumbufu unaoweza kujitokeza," amesema Mwambene.