Home | Terms & Conditions | Help

May 18, 2024, 9:31 pm

NEWS: WAZIRI WA ARDHI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA WIZI

Aliyekuwa waziri wa Aridhi na Makazi nchini Kenya Amos Kimunya (kushoto) na watuhumiwa wengine wawili leo wameburuzwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya ufisadi ya kuuza shamba la umma lenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.14.

Kimunya ambaye alikuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la 12, pamoja na washukiwa wengine wawili wamejisalamisha kortini baada ya Mahakama Kuu kuamuru washtakiwe upya.

Bw Kimunya, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ardhi Bi Lilian Wangiri na Bw Junghae Wainaina walijisalamisha mbele ya hakimu mkuu mahakama ya kesi za ufisadi Milimani, Nairobi Bw Lawrence Mugambi.

Kimunya, Lilian na Wainaina wataanza kujitetea Oktoba 31, 2022 mbele ya hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko aliyeteuliwa kupokea tetezi zao na Bw Mugambi.

Watatu hao waliagizwa na Jaji Esther Maina mnamo Septemba 29,2022 wafike mbele ya Bw Mugambi wajitetee katika kesi waliyoachiliwa miaka miwili iliyopita.

Jaji Maina alikubaliana na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) katika rufaa aliyokata kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuamuru Kimunya,Lilian na Junghae wajitetee katika kesi iliyowakabili ya ulaghuzi wa mali ya umma.

Bw Kimunya atajitetea katika mashtaka saba yanayomkabili ilhali wenzake wawili watajitetea katika mashtaka nane dhidi ya kila mmoja.

Walipojisalamisha kortini, washtakiwa hao waliomba waachiliwe kwa dhamana.

Bw Mugambi alimwachilia Bw Kimunya kwae dhamana ya pesa tasilimu Sh700,000.

Na wakati huo huo, Bw Mugambi aliwaagiza Lilian na Junghae walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni kila mmoja.

“Dhamana ni haki ya kila mshtakiwa. Basi nitawaachilia kwa dhamana kama ifuatavyo – Kimunya Sh700,000, Lilian Sh1 milioni na Junghae Sh1 milioni pesa taslimu. Mtafika kortini tena Oktoba 31, 2022 kuanza kujitetea kama ilivyoamriwa na Jaji Maina mnamo Septemba 29, 2022,” Bw Mugambi aliagiza.

Bw Junghae Wainaina alikuwa mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo ya Midlands Limited iliyotunukiwa shamba hilo la Sh60 milioni, Bw Kimunya alipokuwa Waziri wa Ardhi.

Bw Kimunya aliye pia mbunge wa zamani wa Kipipiri ndiye mwanasiasa wa kwanza mwenye ushawishi mkubwa katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta kushtakiwa kwa ufisadi.

Bw Kimunya aliachiliwa na hakimu mkuu Felix Kombo mnamo Mei 2020.

Shamba hilo lililopelekea watatu hao kushtakiwa ni la ekari 25.

Kampuni ya Midlands ni ya umma na ilibuniwa 1987 na iko na wanachama 1,496 miongoni mwao hayati Mwai Kibaki na marehemu Lucy Kibaki.

Wanachama wengine wa kampuni hiyo ya Midlands ni makundi ya kujisaidia na kampuni katika eneo la Kinangop.

Shamba hilo lilinuiwa kukuzwa viazi.